Samatta awapa somo wachezaji wa Tanzania

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars  na klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji Mbwana Samatta amewataka wachezaji wenzake wa Tanzania kutumia vizuri fursa chache  zinazopatikana wakati wanapopata nafasi za kwenda kufanya majaribio nje ya nchi kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa.

Akiongea na Goal  Samatta amewataka wachezaji wenzake kujituma na kutumia uwezo wao wote ilikuweza kufuzu majaribio wakati nafasi zinapopatikana.

"Najua siyo kazi rahisi kupata nafasi na kufanikiwa kufuzu majaribio lakini nawaomba wakati zinapotokea nafasi za kwenda kufanya majaribio wahakikishe wanazitumia vizuri kwa kupambana hadi mwisho na siyo kukubali kirahisi ukizingatia nafasi hizo hazipatikani kirahisi,”alisema Samatta.

Samatta amesema kuwa wakati wote mchezaji anatakiwa kuwa tayari kwa mapambano bila kuzingatia ni wapi anacheza na inapotokea ameshindwa  kufuzu majaribio na kurudi nyumbani asikate tamaa ua  kubweteka bali kinachotakiwa ni kujipanga na kuweka mikakati ya kuanza  mipango ya kutafuta nafasi za kwenda kucheza Ulaya.